SOMA:Tamko la Jumuia na Taasisi za Kiislaam nchini Tanzania.

Friday May 01, 2015 - 22:58:59
14463
Super Admin
TAMKO LA JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAM TANZANIA JUU YA KADHIA YA KUFUNGA MADRASSA NA UKAMATAJI WA MASHEIKH NA KUNYIMWA DHAMANA.


Kwa muda sasa jeshi la polisi limekuwa linaendesha vita dhidi ya madrasa na masheikh Tanzania kwa kuvamia na kukamata watoto na waalimu wa madrassa, kuvamia misikiti na kukamata masheikh na maimamu wa misikiti, kuvamia misikiti na kudai kukamata milipuko katika mazingira yanayoleta shaka na utata, na viashiria vya vitendo vya kibaguzi katika kushughulikia masuala yanahusiana na viongozi wa dini mbalimbali hapa nchini. Baadhi ya viongozi wa serikali ngazi za wilaya, mikoa na taifa wamekuwa wakiungana na jeshi la polisi katika harakati hizo ambazo zinaathiri uislamu na waislamu nchini kwa namna mbalimbali kama tutakavyoonyesha hivi punde.

Tuhuma wanazokuwa wanatoa polisi kuhalalisha harakati za uvamizi na kamata kamata ni pamoja na madrassa na masheikh kufundisha dini ya kiislamu kinyume cha sheria; kukusanya watoto na kuwafundisha elimu ya dini kinyume cha sheria na katika mazingira yasiyofaa; pia inadaiwa kufundisha na kufanya mazoezi yanayoendana na ugaidi; kinyume cha sheria; kuwepo kwa taarifa za watu wenye milipuko misikitini; na kutuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi.

Kule Moshi mkoani kilimanjaro watoto na walimu wa madrassa wamekamatwa kama ilivyokuwa mtwara Mwalimu wa madrassa bado anashikiliwa na polisi kwa kuwa na watoto akiwafundisha dini ya kiislamu na Dodoma watoto wa madrassa, waalimu wao na mwenye nyumba wanakofundishia watoto dini ya kiislamu walikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi kuhojiwa na kuchukuliwa alama zao za vidole kama ilivyo kwa wahalifu.

Huko kilombero mkoani morogoro watu waliingia msikitini saa tisa za usiku na muda mfupi baadae polisi wakaja na kuvamia msikiti kwa namna ambayo inatia shaka kwamba polisi walifahamu watu hao wametoka wapi au walihusika kwa nia ya kuchafua hadhi ya msikiti na uislamu. Watu waliokamatwa si wenyeji wala wakaazi wa eneo linalotumia msikiti huo. Hilo halikutajwa na polisi wala kiongozi yeyote wa serikali.

Wengi wa waliokamatwa wamekuwa wakihamishwa kutoka kituo kimoja cha polisi hadi kingine, kambi moja ya mahojiano na mateso hadi nyingine, mahala hapa kwenda pale na mkoa mmoja hadi mwingine, wakihojiwa na watu/maafisa mbalimbali bila kupewa haki ya usaidizi au uwepo wa ndungu au wanasheria.

Matendo na maneno yanayotendwa na kutamkwa na viongozi wa serikali na polisi kuhusu uislamu, waislamu, madrassa, misikiti, elimu ya dini ya kiislam inaonyesha nia mbaya iliyopo dhidi ya dini yetu.

Madrassa ni sehemu rasmi ya kufundisha na kutoa elimu ya uislamu kama dini na mfumo wa maisha kamili ya mwanadamu. Kimfumo ni kwamba Madrasa nyingi aghalabu huwa kwenye

misikiti, karibu na misikiti, nyumbani kwa masheikh au nyumbani kwa maimamu. Madrasa hizi zimekuwepo tangu uislamu uanze ikiwa ni mfumo wa kufundisha na kupata elimu ya dini ya kiislamu na ni sehemu ya kueneza dini inayotambulika na kulindwa na katiba yetu, sheria zetu na taratibu za maisha ya kawaida ya jamii yetu.

Madrasa za bweni zimekuwa zikichukua na kupokea mayatima na watoto kutoka familia duni na wasiojiweza na walio katika mazingira hatarishi na watoto wa mitaani na wengineo wenye kutaka kujua dini. Mzigo wa kulea na kuweka mazingira mazuri watoto hawa ni jukumu la serikali. watoto hawa wanakamatwa usiku wa manane wamelala, bila hati ya kupekua na kukamata, wanatishwa (terrorised) na polisi. Kimsingi sio suala la kipolisi bali suala la ustawi wa jamii na maafisa elimu kwenda kukagua na kushauri namna kuboresha. maana yote yanafanyika kwa nia njema, kwa uwazi na hakuna aliyelalamika juu ya kinachofundishwa kwenye madrassa hizo; ni polisi tu ndio wanatuhumu kufundisha elimu ya dini ya kiislamu kuwa ni kinyume na sheria.

Mkakati na operesheni ya polisi inakiuka haki nyingi za binadamu, haki za kikatiba, haki za kisheria, utu, ni uchochezi dhidi ya waislamu kwa kuwafanya wachukiwe na jamii, na waonekane waislamu si waaminifu, hawapendi amani, kwamba dini ya uislamu haipaswi kufundishwa na kana kwamba kuna sheria imetungwa na nchi yetu inayoonyesha namna na nini cha kufundisha katika dini ya uislamu. Kimsingi waislamu, maisha yao, taasisi zao, mfumo wao wa imani na ufundishaji havijapata ulinzi kwa serikali na vyombo vyake vya dola. Wajibu wa serikali kutulinda haujatimizwa bali tunawekwa katika mazingira ya hatari katika kushambuliwa kwa maneno na kivitendo nchini na kimataifa.

kwa matendo na matamko ya polisi na viongozi wa serikali, ni dhahiri sasa tumekosa na tunaendelea kukosa haki ya kuishi, kuwa huru na kulindwa na sheria na serikali (Ibara 12, 14 & 29(2) ya katiba); haki ya kuwa sawa mbele ya sheria na kupata haki bila ubaguzi (Ibara 13); Haki ya kuishi kama mtu huru (ibara 15); Haki ya faragha na usalama (ibara 16); Haki ya kuamini dini, kuisoma, kuielewa, kuieneza na makuzi kwa mujibu wa dini ya uislam bila kuingiliwa(ibara 19); haki ya watoto kutobughudhiwa na kutishwa usiku wa manane kinyume na sheria ya watoto ya mwaka 2009 na makuzi yao; kinyume na kanuni za utawala bora; na haki ya kutokuwa kizuizini kwa sababu yoyote kwa zaidi ya masaa 24 bila amri ya mahakama;

Polisi na viongozi wa serikali kwa matendo yao, matamko yao, na kwa taathira ya wanayoyafanya dhidi ya waislamu na waislamu imewagawa na inaendelea kuwagawa watanzania kwa misingi ya imani za dini kinyume kibisa cha misingi imara ya nchi hii.

Madrassa zinaendeshwa na hazifungwi na sheria ya elimu na wala sera ya elimu ya Tanzania. Sheria na sera ya elimu haziwezi kuelekeza madrassa ziweje na zifundishe nini kwa sababu masuala ya dini yako nje ya shughuli za serikali kikatiba na kisheria. Kama ambavyo serikali haingilii mikutano na mafundisho ya dini ya kikristo katika jumuiya ndogondogo

zinazofanyika mitaani na majumbani hivyohivyo ndivyo serikali inapaswa kufanya kwa madrassa.

KUKAMATWA NA KUNYIMWA DHAMANA KWA MASHEIKH

Viongozi wa dini ya kiislamu wakikamatwa kwa tuhuma za makosa yanayodhaminika polisi wamekuwa wakiwanyima dhamana bila sababu za msingi, kudhihakiwa na kunyanyaswa kiimani zao na pale wanapopelekwa mahakamani imekuwa ni kanuni na desturi ya Mkurugezi wa Mashtaka Nchini (DPP) na ofisi yake kupeleka pingamizi la dhamana bila kutaja sababu zozote. Kanuni na desturi hiyo imekuwa ikifaa kutumika tu kwa waislamu. DPP ambaye ni mkristo hajathubutu kutumia mamlaka ya kuzuia dhamana kwa wengine nje ya waislamu.

Sheikh Ponda kwa sasa yupo ndani sio kwa sababu ya amri yoyote ya mahakama yoyote bali ni kwa sababu ya matakwa ya DPP kupendezwa na kuendelea kwake kuwa mahabusu kwa kipindi ambacho ni zaidi ya adhabu kwa miaka miwili sasa. Huku Askofu Gwajima na viongozi wengine wakiachwa huru kufanya wanachotaka, kutamka wanachotaka, kuhamasisha kuipigia kura ya hapana katiba pendenkezwa kinyume na sheria, kukusanyika vituo vya polisi kama wapendavyo wakishinikiza kuachiwa huru viongozi wao, nk. yote hayo yamefanyika na yanaendelea kufanyika polisi wakiona na wanawalinda na kuwawekea mazingira ya kufanya hayo, hawakatazwi bali hubebembelezwa kwa kutangazwa kwenye vyombo vya habari waende wenyewe polisi. Viongozi hao wakikristo hawawanyimi dhamana wahusika na zaidi wanajidhamini wenyewe, na wanapofikishwa mahakamani DPP hafanyi chochote kanakwamba hayupo kabisa zaidi ya kusema hana pingamizi na dhamana. Hii ni double standard; ofisi za umma zinahudumu na kutekeleza sheria kwa upendeleo na ubaguzi wa wazi kabisa dhidi ya waislam.

kwa ujumla picha inayotolewa na polisi na viongozi wa serikali ni kwamba waislamu na taasisi zao, mifumo yao ya dini ni ya daraja la chini.

kwa bahati mbaya na kwa makusudi hakuna kiongozi wa serikali ameongea, kuhoji, kuonya na kutafakari juu ya ukweli na usahihi wa habari zinazoathiri waislamu na taasisi husika kitu kinachotuaiminisha kuwa ni mkakati mahsusi.

kwa taarifa hii umma wa waislamu unategemea na unataka serikali, Mkuu wa Polisi (IGP), DPP na Kila kiongozi aliyehusika na anayehusika kushiriki au kutekeleza harakati dhidi ya umma wa waislamu na taasisi zao kuchukua hatua za kujirekebisha na kuacha kuchochea jamii dhidi ya uislamu; watende kazi na kuhudumia umma wa uadilifu, maadili, kwa mujibu wa sheria na katiba; wasifanye kazi kwa upendeleo na kuasisi matabaka katika jamii. wafanye kazi kwa upendo na weledi.

HIVYO BASI TUNATAMKA YAFUATAYO.

1.Serikali iombe radhi kwa waislam kwa vitendo vya jeshi la polisi kunyanyasa na kuzihujumu madrassa ambazo ndicho kiini cha elimu ya dini kiislam na maadili mema kwa jamii.

2.Serikali iache mara moja kuzivamia kuziandama madrassa na kuwaweka mahabusu watoto wadogo wa madrassa kwa kisingizio cha madrassa kutokusajiliwa ilihali hakuna sheria wala sera ya elimu inayotaka madrassa zisajiliwe.

3.Serikali iache kuzivamia na kuziandama madrassa kwa hoja kuwa ziko katika mazingira duni ilihali ziko shule za serikali na vituo vya watoto yatima vilivo katika hali duni kuliko madrassa zetu.

4.Serikali itoe dhamana kwa masheikh walioko mahabusu kama inavofanya kwa maaskofu na wachungaji walioshtakiwa mahakamani.

5.Jeshi la polisi liwaachie au kuwapa dhamana masheikh, maustadhi na maimamu waliokamawta sehemu mbalimbali nchini na ambao wako katika mikono mwa polisi kwa muda mrefu bila ya kufikishwa mahakamani.

MWISHO.

Mnamo tarehe 15/05/2015 endapo hayo tulioyatamka hapo juu yatakuwa hayajapata ufumbuzi kutoka kwa serikali tunatangaza rasmi tutafanya maandamano makubwa siku hiyo kwa waziri wa mambo ya ndani.

 

Imetolewa na JUMUIYA NA TAASISI ZA KIISLAMU (T)

 

...........................

Sheikh. Mussa Kundecha

Mwenyekiti.

Related Items

Update cookies preferences